Wachuuzi wa vyakula vilivyochemshwa mjini Kisumu wametakikwa kuzingatia usafi kwenye maeneo wanayofanyia kazi zao ili kupunguza uwezekano wa kupatwa na maradhi ya kipundupindu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu wa Katibu wa Wizara ya Afya mjini, Sophia Nduti amewaambia wachuuzi Kisumu kusafisha maeneo ya kazi na kufunikwa kwa vyakula vilivyopikwa ili kuzuia nzi kusambaza uchafu kwa vyakula, akiwataka kuzingatia sheria za usafi kwa kujenga vyumba vya kuuzia.

“Kuuza vyakula vilivyopikwa hapa nje ni hatia kufuatia sheria za afya. Ni vyema kujenga vyumba hata vibanda kwa utunzi mzuri wa vyakula kwa afya ya uma,” alisema Nduti.

Alisema kuwa amri iliyokua imetolewa awali kupiga marufuku uuzaji wa vyakula kwenye maeneo yaliyowazi bado itarejelewa iwapo wachuuzi hao hawatazingatia sheria za afya kikamilifu.

“Tunaendelea kuangalia uwezekano wa kuhatarisha afya ya wananchi na iwapo hatari itakua juu, basi hatuna budi kuwafungia hadi mtakapotekeleza masharti,” alisema afisa huyo wa afya alipotembelea soko la Kibuye mnamo Jumatano.

Wakijitetea kwa afisa huyo, baadhi ya wachuuzi hao walisema kuwa wanajaribu upande wao kuhakikisha usafi wakati wa kazi, lakini wakanyoshea kidole cha lawama baraza la mji ambalo walisema huacha kwa muda mwingi taka zilizokusanywa hali ambayo inachangia mazingira kuwa chafu mno.

Mji wa Kisumu umebeba idadi kubwa ya wachuuzi wanaotegemea biashara hiyo ambapo wengine wanauza kwa njia ya kutembeza chakula huku na kule mjini, hali ambayo inaongeza hatari ya kuathirika kiafya.