Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyabiashara katika soko kuu la Eldoret wameelezea hofu ya kutokea mkurupuko wa ugonjwa katika soko hilo kutokana na murundiko wa taka sokoni humo.

Wanabiashara hao walisema hali ya usafi sokoni humo imekuwa mbaya zaidi msimu huu ambapo mvua ya El~Nino imeanza kushuhudiwa mjini humo.

Wengi wa wafanyabiashara hao ambao wanauza mboga na matunda wamekashifu utawala wa kaunti hiyo kwa kuzembea kusafisha soko hilo.

Kwa pamoja walitoa wito kwa idara husika kujizatiti kuboresha mbinu ya uzoaji taka.

Wanabiashara hao walionya kuwa ikiwa hali katika soko hilo itaendelea kuwa hivyo watasusia kulipa ushuru.

Hata hivyo naibu gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Daniel Chemno alisema kila juhudi zinafanywa ili kuimarisha usafi sokoni humo ambapo aliwataka wachuuzi husika kushirikiana na idara ya uzoaji taka mjini humo kudumisha usafi wa soko hilo.

"Tayari wizara ya mazingira na maji katika kaunti hiyo imeanza kutoa zabuni ya kuzoa taka na kufungua mitaro ya maji taka kwa makundi ya vijana kama tahadhari ya mapema ya kukabiliana na thari za mvua ya El~Nino," alisema Chemno.

Waziri wa mazingira na maji Mary Njogu alisema kila juhudi zinafanywa ili kuimrisha usafi mjini Eldoret.

Njogu alisema kuna mpango ya kuongeza mabiba zaidi ya kukusanya taka katika masoko yote ya kaunti hiyo.