Wakaazi wajulikanao kama Bondeni Community Empowerment Program wameonya mawakala dhidi ya kuingilia na kuligawa soko ambalo linanuia kujengwa Ziwani viungani mwa mji wa Nakuru.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wao Maurice Otieno ni kuwa ipo haja wenyeji wanaoishi eneo hilo kupewa kipaumbele kabla ya kuwapa fursa wachuuzi wengine kutoka nje.
Kupitia kwa mwenyekiti huyo wa jumuiya hiyo kutoka maeneo ya Bondeni,Kanyoni, Kambi Somali, Kisulisuli, Lumumba, Abong’oloya, Kona tatu, KFA na Pyrethrum yaliyoko viungani mwa mji wa Nakuru amewataka viongozi katika kaunti ya nakuru kitilia maanani jambo hilo wala wasipotoshwe na wale ambao wanajitakia makuu.
Mwenyekiti huyo amedokeza kuwa eneo hilo la ziwani litajengwa soko ambalo ni katika mapatano ya ukodishaji kati ya shirika la reli la kenya pamoja na serikali ya kaunti ya nakuru kwa muda wa miaka hamsini.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amedai kuwa iwapo matakwa yao kwa mujibu wa katiba hayatazingatiwa, watalazimika kuandamana.
Aidha baadhi ya wanachama wa kamati ya jumuiya hiyo inayowakilisha mitaa hiyo tisa wamesisitiza na kusema kuwa hawataruhusu yeyeote kutoka nje kuja na kuwahujumu.
Hata hivyo jumuiya hiyo imeahidi kufanya kazi na serikali ya kaunti ya nakuru kwa manufaa wa jimbo nzima.