Wachuuzi katika mji wa Kisii wameonywa dhidi ya kuchafua mazingira yao ya kufanyia kazi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza kwenye afisi yake, waziri wa afya katika kaunti ya Kisii Bi Sarah Omache amewataka wachuuzi, hasa wanaopika na kuuza vyakula, kudumisha viwango vya juu vya usafi kama njia moja ya kujikinga na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama kipindupindu.

“Nawaomba wachuuzi kudumisha usafi kwani ni njia moja ya kujikinga na magonjwa yanayosababishwa na uchafu,” alisema Omache.

Halikadhalika, aliongezea kuwa huu ukiwa ni msimu wa mvua katika mji wa Kisii, ni vyema wachuuzi kuwa makini na kudumisha usafi kwani hali ya anga ni murwa kwa magonjwa.

“Huu ukiwa ni msimu wa mvua na baridi, magonjwa yana asilimia kubwa kuchipuka,” aliongezea.

Vilevile, amewaonya wale ambao hawatazingatia usafi kuwa huenda wakachukuliwa hatua za kisheria.

“Sheria ipo tayari kuwadhibu wale watakaokiuka onyo hili na kuhatarisha maisha ya wananchi kiholela,” alisema.

Ni siku za hivi punde ambapo kumekuwa na kuenea kwa wachuuzi hasa kwenye maeneo ya taasisi kama shule, na huenda maisha ya umma ikawa hatarini iwapo hali ya usafi haitazingatiwa.