Makundi ya wazazi pamoja na wafanyibiashara wa vitabu katika kaunti ya Nakuru wamesihi serikali kumaliza mgomo wa walimu huku wakiyataka makundi ya kutetea haki za walimu kulegeza misimamo yao mikali ili kupisha mazungumzo kati yao na serikali.
Matokeo mabaya ya mitihani ya kitaifa huenda yakashuhudiwa mwakani iwapo serikali na vyama vya kutetea haki za walimu hawatasikizana na kufanya maafikiano ili kumaliza mgomo unaoendelea na ambao unatatiza hali ya masomo katika shule za umma.
Peter Mburu ambaye amewahi kuhudumu kama mtetezi wa maslahi ya walimu katika tawi la Nakuru, amesema ni sharti kuwe na mkataba kati ya serikali na wafanyikazi wake ili kupunguza migomo ya kila mara.
Amesema kuwa kwa miaka mingi sasa serikali imekuwa ikiwapa waalimu ahadi ya kuongezwa mishahara pamoja na marupurupu mengine lakini serikali huzikiuka mkataba na kudinda kuongeza mishahara.
Mburu ambaye amesema migomo ya wafanyikazi husababisha madhara ya kiuchumi kwa taifa, amesihi serikali kutimiza ahadi zake ili migoma za mara kwa mara zikomeshwe.
“Ni hofu kuona kuwa wanafunzi katika shule za umma wanaendelea kuteseka huku makundi ya kutetea walimu pamoja na serikali wakiendelea kutofautiana,” alisema Mburu.
Mburu alidokeza kuwa shule nyingi za umma zimefeli kumaliza mwongozo wa elimu ( silabasi) kwa sababu ya mgomo ya kila mara ya walimu pamoja na migomo ya wanafunzi katika baadhi ya shule.
Aidha Mburu amedokeza kuwa mfumo wa elimu bila malipo umekubwa na misururu ya migomo ya walimu huku akisema huenda viwango vya elimu vikadorora iwapo hatua mahubuti haitachukuliwa.