Kamati ya kudhibiti ongezeko la ugonjwa wa ukimwi eneo bunge la Changamwe, 'Constituency Aids Control Committee' imeunga mkono takwimu zilizotolewa na baraza la kitaifa kuwa zaidi ya asilimia hamsini ya wanaougua ugonjwa huo ni vijana ambao wamebalehe.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na waandishi wa habari, mwenyekiti wa kamati hilo Maurice Ochieng' amesema kuwa takwimu hizo zimechangiwa pakubwa na kutowajibika kwa washikadau mbalimbali wa elimu ikiwemo walimu, wazazi na hata viongozi wa kidini ambao amewataja kuwa na jukumu la kueneza mafunzo ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Ochieng' amesema kila wanapotayarisha takwimu za eneo bunge la Changamwe kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi, idadi kubwa ya vituo vya afya eneo hilo huandikisha ongezeko la wanaoathirika na ugonjwa huo.

Ochieng’ ambaye pia amekuwa akihudumu kama mjumbe wa kueneza namna ya kujikinga na ugonjwa huo, alikiri kuwa kutengwa kwa baadhi ya vijana katika jamii pia kumechangia ongezeko hilo.

Alisema kuwa hali hiyo humlazimu kijana kutafuta hela kwa njia zozoto na mwishowe huishia kupata wanaume ama hata vijana wenzake na kuishia kushiriki ngono bila ya kutumia kinga.

Ikumbukwe kuwa hapo awali, Ochieng’ aliwaomba wazazi, viongozi wa kidini pamoja na wale wa jamii ikiwemo walimu kuwapa mwelekeo watoto wao ili waweze kujikinga dhidi ya ugonjwa huu ambao unaendelea kuwakumba vijana ambao amewataja kama taifa la baadae.

Takwimu hizo zilitolewa na mkurugenzi wa kongamano la kitaifa la walimu wakuu wa shule za msingi Nduka Nzioki.