Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa amewakashifu wadau katika sekta binafsi kwa kuendeleza ufisadi bungeni.
Aden Duale amewakosoa wadau hao kwa kuwahonga wabunge ili kupitisha sheria zinazowapendelea.
Akiwahutubia wafanyabiashara mjini Mombasa, Duale amewataka wadau hao kukoma kuwapa wabunge mamilioni ya pesa ili kupitisha sheria na miswada aliyoitaja kama isiyokuwa na muhimu.
“Wadau hao wamekuwa wakitumia fedha kushawishi wabunge kupitisha miswada mipya pamoja na kubadili sheria zilizopo, ili kunufaisha kampuni na biashara zao,” alisema Duale.
Aidha, amesema kwamba wadau hao wa sekta binafsi nchini wanampa spika wa bunge wakati mgumu wa kusitisha sheria mbaya.
“Tabia hii inampa spika wa bunge wakati mgumu wa kuhakikisha hakuna sheria za upendeleo zinapitishwa bungeni,” alisema Duale.
Duale alisema kuwa atahakikisha tabia hiyo inasitishwa na wanaohusika wanakabiliwa kisheria.
“Tutawakabili wadau na wabunge wanaoendeleza ufisadi bungeni na kuwafungulia mashtaka,” alisema Duale.