Muungano wa wamiliki wa matatu nchini umeunga mkono sheria mpya za barabarani zilizozinduliwa na mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, katibu mkuu wa muungano huo Sammy Gitau ameitaka NTSA kuimarisha mbinu za kuwachukulia hatua madereva watakaokiuka sheria hizo ili kutowapotezea muda wasafiri.

“NTSA sharti izindue mbinu mwafaka zitakazohakikisha kuwa kesi za wanaovunja sheria zinatatuliwa kwa muda unaofaa ili kusiwe na mrundiko wa kesi katika mahakama ya kusuluhisha mgogoro barabarani,” alisema Gitau.

Aidha, Gitau amewataka madereva kutotoa hongo kwa maafisa wa polisi wanapopatikana na makosa, akisema hatua hiyo inachangia kuongezeka kwa ufisadi katika sekta ya uchukuzi.

“Wakenya lazima tubadilishe hulka yetu. Tabia ya kuchukua hongo inazamisha taifa hili. Wewe kama dereva ukipatikana na hatia, lipa faini zinazohitajika, usimpe afisa wa polisi hongo kukwepa mkondo wa sheria,” alisema Gitau.

Gitau ambaye pia ndiye mwenyekiti wa wamiliki wa matatu mjini Mombasa, vilevile ametoa wito kwa madereva hasa wa magari ya uchukuzi kuzingatia sheria za barabarani ili kuzuia ajali za mara kwa mara.

Kulingana na sheria hizo mpya, madereva watakaovunja sheria za barabarani watatozwa faini isiyozidi shilingi elfu 10 ambayo italipwa papo kwa hapo kwa maafisa wa usalama.