Waziri wa utalii nchini Najjib Balala amesaidia pakubwa katika kuimarisha sekta ya utalii iliyokumbwa na msukosuko na kupelekea wageni wengi kuzuru eneo la Pwani tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulingana na Chama cha Watalii nchini yaani ‘Kenya -coast tourist Association’, hatua ya Waziri Balala ya kuzuru hoteli na maeneo mbalimbali ambayo ni kivutio cha watalii imepelekea wageni wengi kuwa na imani na utenda kazi wa serikali.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mkurugenzi mkuu wa Chama hicho Bi Millicent Odhiambo amesema kuwa iwapo Waziri Balala atazidisha ushirikiano na wadau wa sekta ya utalii kubaini changamoto zinazoikumba sekta hiyo basi itaimarikia zaidi.

“Tunaunga mkono juhudi za Waziri Balala na tuna imani kwa ushirikiano na juhudi zaidi sekta ya utalii itaimarika nchini na hususan eneo la Pwani,” alisema Odhiambo.

Ameitaka wizara hiyo ya utalii kuhakikisha kuwa inaliangazia zaidi eneo la Pwani kama kitovu cha utalii ili kuimarisha hata uchumi nchini.

Hivi majuzi, waziri huyo wa utalii alizuru maeneo mbalimbali ya Pwani ikiwemo Kaunti ya Lamu ili kutathmini hali halisi ya mahoteli na vituo vingine vya utalii katika Ukanda wa Pwani.

Picha: Waziri wa utalii nchini Najjib Balala akifanya vikao na kuboresha sekta ya utalii na wadau wa sekta hiyo Mombasa. Utalii umeimarika tangu achaguliwe kuwa waziri, kulingana na washikadau.