Wadau katika sekta ya utalii nchini wamehimiza umuhimu wa kuboresha utalii wa kinyumbani ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaimarika zaidi.
Mwenyekiti wa Chama cha Utalii nchini Mohamed Hersi, amesema kuwa hatua ya wadau wengi wa sekta hiyo pamoja na Wakenya kutoangazia utalii wa kinyumbani imechangia kuwepo na changamoto kubwa katika sekta hiyo.
Akiwahutubia wanahabari siku ya Alhamisi, Hersi alisema kuwa iwapo miundo msingi itaboreshwa zaidi, basi sekta hiyo itaimarika kwa kiasi kikubwa.
Hersi aidha aliishinikiza serikali kukabiliana na misongamano katikati ya miji mikuu.
"Kuna umuhimu wa wadau wa sekta ya utalii, serikali kuu na zile za kaunti kuangazia zaidi utalii wa kinyumbani kama njia moja wapo ya kuimarisha sekta hii na kuinua uchumi wa nchin,” alisema Hersi.
Wakati huo huo, amependekeza safari za moja kwa moja kutoka mataifa ya magharibi hadi Mombasa kuidhinishwa ili kuwavutia watalii wengi zaidi humu nchini na hususan eneo la Pwani.
Hersi pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano thabiti baina ya serikali kuu, zile za kaunti na wadau wa sekta ya utalii ili kukuza uchumi wa nchi.