Shirika lisilokuwa la kiserikali linaloangazia maswala ya maji na mazingira nchini la Maji na Ufanisi, limeishinikiza bunge la kitaifa kujadili kwa kina sheria ya maji na kuipitisha ili Wakenya wazidi kupata maji safi hata mashinani.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Ukunda, afisa mkuu wa Shirika hilo kanda ya Pwani Bi Hamisa Zaja, amesema kuwa iwapo bunge la kitaifa litapisha sheria hiyo ambayo ingali inapigwa msasa bungeni, basi tatizo la uhaba wa maji safi na mazingira bora mashinani litatauliwa.
Zaja alisema kuwa ugatuzi unafaa kupewa msukumo zaidi katika kuhakikisha kuwa maswala kama hayo yanapewa kipau mbele, kutokana na kuwa maji ndio jambo la muhimu kwa binadamu
Aidha, afisa huyo alishinikiza viongozi bungeni kuliwajibikia swala hilo.
Kwa sasa wadau hao wa sekta ya maji wanaendelea na vikao vya mazungumzo katika hoteli moja mjini Ukunda, kubaini jinsi ya kuliangamiza tatizo la uhaba wa maji safi, mazingira bora, pamoja na uimarishaji wa utumizi wa maji ya visima katika ukanda wa Pwani.