Wahudumu wa bodaboda Soy wamelalamikia kunyanyaswa kwao na watu 'wanaoona' wana nguvu.
Kulingana na wahudumu hao, ajali nyingi wanazopata eneo hilo huwa hazishughulikiwi ipasavyo kisheria.
Hii ni baada ya mmoja wao kugongwa na gari la polisi na baadaye kusemekana kwamba aligongwa na pikipiki nyingine.
Muungano wa wanabodaboda hao kupitia mwakilishi wao Patrick Omar, wamesema kwamba wanapitia changamoto nyingi ambazo nyingi zinasababishwa na kuzembea kwa maafisa wa polisi.
Akizungumza kwa mazishi ya mmoja wao aliyegongwa na gari hivi majuzi, Omar amewahimiza wanabodaboda kuwa waangalifu mwaka huu unapoanza ili kupunguza idadi ya watu wanaofariki kupitia ajali za barabara.
Aidha, bodaboda hao wametishia kwamba iwapo sheria haitafuatwa na wenzao kupata haki, basi watachukua hatua zao wenyewe.
“Tutajipanga vilivyo iwapo sheria itatuumiza sisi wanyonge,” alisema Omar.
Waliongeza kuwa, huduma za hospitali ya Likuyani ziongezwe na kutiiliwa maanani.
“Wale majamaa wanafanya kazi kwa hospitali ya Likuyani hawafanyi kazi inavyostahili,” walisema huku wakiongeza kwamba vifaa vyafaa kuongezwa katika hospitali hiyo kwa huduma za dharura kwa wananchi.
Aidha, bodaboda hao wametishia kuchukua hatua mikononi mwao na kukabiliana na madereva wanaowasababishia ajali waendeshaji wa bodaboda.
“Tutafanya kila tuwezalo kwa sababu kesi hizi zikiingia kotini huwa hazishughulikiwi ipasavyo,” alisema Omar.