Mwakilishi wa wadi ya Bogetenga, Kaunti ya Kisii, Rueben Moreka, ameahidi kuwapeleka waendeshaji bodaboda katika wadi yake kupata mafunzo ya jinsi ya kuendesha pikipiki kwa kutumia pesa za basari.
Hii ni baada ya kubainika kuwa wengi wao hawana mafunzo halisi ya kuendesha bodaboda jambo ambalo huwapelekea kusababisha ajali kila mara wanapofanya uchukuzi barabarani.
Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Ndonyo, mwakilishi huyo aliahidi kuzitumia pesa za basari kuwapeleka waendeshaji bodaboda shuleni ili kupata mafunzo kikamilifu.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo aliwafadhili waendeshaji bodaboda hao Sh20,000 za kufungua hazina ya kuweka pesa zao kila siku ili ziwakimu katika maisha ya kesho.
“Nitatumia pesa za basari ili muende shule kwani wengi wenu katika wadi hii hamna mafunzo ya kuendesha bodaboda,” alisema Moreka.
Wahudumu hao wa bodaboda walimpongeza mwakilishi huyo wa wadi kwa kuwaahidi kuwapeleka shuleni na kuwasaidia kufungua Sacco yao ili waweze kujiendeleza katika maisha yajayo.
“Tunaona huyu mwakilishi wetu anatujali sana maana ametukabidhi Sh20,000 na tumefungua akaunti ya Sacco na tutajiendeleza kwani tutakuwa tukiweka pesa zile tunatengeneza kila siku,” alisema Brian Bosire, mwendeshaji bodaboda.