Wanaoendesha Bodaboda mjini Chemelil wamelalamikia vikali kudorora kwa usalama kwenye barabara za eneo hilo haswa nyakati za usiku huku wakinyoshea kidole cha lawama vyombo vya usalama katika eneo hilo.
Wakiongea siku ya Jumapili katika uwanja wa Shule wa Achego Wilayani Muhoroni kwenye mkutano wao wa kila mwezi wa wanachama wa Bodaboda wa kuchangisha pesa za hazina ya msiba, Waendeshaji Bodaboda hao kupitia kwa mwenyekiti wao Dalmas Aroko, walimtaka Mkuu wa Polisi katika kituo cha Polisi cha Chemelili kuamuru kuanzishwa kwa msako nyakati za usiku kwenye barabara za eneo hilo ili kuwakabili wahuni wanaowahangaisha usiku wakiwa kazini.
“Tunataka barabara ya kuelekea Kopere hadi Songhor na ile ya Muhoroni na Tamu kuwekwa ulinzi mkali kupitia msako nyakati za usiku ili tuepuke kushambuliwa mara kwa mara,” alisema Aroko.
Aidha, wanachama hao walitaka wenzao kwenye kazi hiyo katika maeneo hayo pia kuzingatia masaa ya kazi, wakisema kuwa kuendelea na kazi hadi masaa yasiyo ruhusiwa pia huchangia uhalifu wakiongeza kuwa hali hiyo huwachanganya maafisa wa usalama kushindwa kupambana na wahalifu ambao hua wanatumia pikipiki kutekeleza uhalifu na kudhaniwa kwamba ni waendeshaji Bodaboda.
“Tunawaonya wenzetu ambao pia hufanya kazi hadi kupitisha masaa yanayo ruhusiwa kisheria kuwa barabarani. Wakipatikana masaa ‘mabaya’ barabarani wasimlaumu yeyote watakapotiwa mbaroni na Maafisa,” aliongeza Mwenyekiti Aroko.
Visa vya kushambuliwa kwa wenye Bodaboda katika eneo hilo na watu wasiojulikana vimeendelea kuongezeka katika siku za hivi majuzi, hali ambayo inaleta uoga miongoni mwa wanaotumia barabara hizo nyakati za usiku.