Mwakilishi wa Wadi ya Manga, Peter Maroro, amewaomba waendeshaji bodaboda kwenye eneo lake la uwakilishi kujiunga kwenye vikundi ili waweze kuomba mikopo kutoka kwenye benki zakibiashara kujiendeleza kimaisha.
Akihutubia wanahabari siku ya Jumatano, baada ya kufungua rasmi afisi za muungano wa wahudumu wa bodaboda Manga, Maroro alisema kuwa wengi wa waendeshaji bodaboda ni waajiriwa wanaolipwa kiwango cha chini cha mshahara hali inayo walazimu kufanya kazi kwa masaa mengi ili kuongeza mapato yao cha kila siku.
"Waendeshaji bodaboda wengi ni waajiriwa wanaopokezwa malipo duni na waajiri wao hali inayo walazimu kufanya kazi kwa masaa mengi ili kujiongezea mapato,” alisema Maroro.
Mwakilishi huyo alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Nyamira kupitia kwa wizara ya jinsia na vijana, imetenga hela kwa minajili ya maendeleo ya vijana na aliwasihi vijana hao kuekeza pesa kwenye mashirika ili waombe mikopo itakayo wawezesha kununua pikipiki zao.
"Serikali ya Kaunti ya Nyamira kupitia kwa wizara ya jinsia na vijana imetenga pesa kwa vijana na nawaomba waendeshaji bodaboda kuchukua jukumu la kujiunga na vyama vya ushirika ili waweze kuomba mikopo itakayo wawezesha kununua pikipiki zao,” alisema Maroro.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda mjini Nyamira Peter Mayaka aliwasihi viongozi mbalimbali wa kisiasa kuwasaidia vijana kuunda vyama vya ushirika vitakao wasaidia kuimarisha maisha yao.
"Ningependa kuwasihi viongozi mbalimbali wa kisiasa wa huku Nyamira kuwasaidia waendeshaji bodaboda kuunda vyama vya ushirika kwa kuwa kupitia vyama hivyo, waendehsaji bodaboda hao wataweza kuimarisha maisha yao,” alisema Mayaka.