Wahudumu wa bodaboda katika eneo la Nyakach, Kaunti ya Kisumu, wamewaonya wenzao katika eneo hilo dhidi ya kukubali kutumiwa na wanasiasa.
Katika mahojiano na mwandishi huyu siku ya Alhamisi mjini Nyakach, wahudumu hao, wakiongozwa na Kevin Omollo, walisema kuwa hawatakubali kuwa vibaraka wa mwanasiasa yeyote.
Walisisitiza kuwa mtazamo wao kwa sasa ni kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo pamoja na kuwapa nafasi ya kusikizwa na kuonekana.
Wahudumu hao walishtumu namna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwatumia na baadae kuwatupilia mbali, huku ahadi za kuwasaidia baadae zikiishia kuzikwa katika kaburi la sahau.
Waendeshaji hao wa bodaboda vile vile wametoa wito kwa wakaazi wa eneo hilo kuzingatia viongozi watakaoleta maendeleo kwenye uchaguzi mkuu ujao.
''Mara hiii sisi tumezinduka na hatutakubali viongozi wa kisiasa kutufanya vile wanavyotaka. Wamekuwa na mazoea ya kututumia lakini kwa sasa hilo litakoma,'' alisema Omollo.