Waendeshaji bodaboda kutoka kaunti ya Nyamira wamelalamikia uongozi wa kaunti hiyo kwa kuwa barabara nyingi ni mbovu na hazipitiki.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongea siku ya Jumatano wakati walikuwa wakiandamana, waendeshaji bobaboda hao katika barabara ya Nyaikuro-Tombe eneo bunge la Kitutu Masaba, waliwalaumu baadhi ya viongozi kwa kutozingatia ujenzi wa barabara katika eneo hilo.

Waendeshaji bodaboda hao walisema kuwa waliamua kuandamana ili kilio chao kisikizwe.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Thomas Arunda, walisema kuwa waliamua kuenda katika maandamano ili kilio chao kisikizwe kwa kuwa wao kama waendeshaji bodaboda wamesumbuka sana hasa msimu huu wa mvua.

Kwa sasa wamemwomba mbunge wa Kitutu Masaba kushughulikia jambo hilo kwa haraka ili kutatua shida hizo kwa haraka.

“Kwa kweli barabara hii haipitiki. Imekua vigumu kufanya kazi kwani pikipiki zetu huaribika kila siku kwa sababu ya barabara hii mbovu. Tunamuomba mbunge wetu ashughulikie jambo hili kwa haraka,” alisema James Mokaya, mwendeshaji bodaboda.

Aidha, wameomba serikali ya kaunti ya Nyamira kushirikiana na serikali kuu na kukarabati baadhi ya barabara ili kurahisisha uchukuzi katika kaunti hiyo.

Kwingineko walisema kuwa wanawake huwa na shida ya kufika hospitalini kwa sababu ya barabara mbovu na biashara imerudi chini.

“Wanawake hasa wajawazito huogopa kupanda pikipiki zetu kwa sababu ya hali mbaya ya barabara. Tunaomba serikali itukumbuke na kukarabati barabara,” alisema Momanyi Joshua.