Share news tips with us here at Hivisasa

Waendeshaji bodaboda wa kituo cha Taraja wadi ya Magenche, eneo bunge la Bomachoge Borabu, Kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya mwakilishi wa wadi hiyo ya Magenche Timothy Ogugu kuwakabidhi mabati ili wajengewe kibanda cha kujikinga mvua inaponyesha na wakati wa jua kali.

Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Taraja, mwakilishi huyo aliwaomba waendeshaji bodaboda hao kuzingatia sheria za barabarani kila siku wanapowabeba wateja.

“Naomba wendeshaji bodaboda wote wa wadi yangu kuwa na heshima miongoni mwo na kuheshimu wateja wenu na muwe mnazingatia sheria za barabara mnapofanya biashara yenu,” alisema Ogugu.

Aidha, mwakilishi huyo aliahidi waendeshaji bodaboda hao kuwapa basari ili kupata mafundisho ya kuendesha pikipiki na kukabidhiwa vyeti vya uendeshaji ambavyo wengi wao hawana.

Waendeshaji bodaboda hao walionekana kufurahishwa na mwakilishi huyo kwani wamekuwa wakisumbuka sana haswa mvua inaponyesha. Walimwomba kuendelea kusaidia waendeshaji bodaboda wengine katika wadi hiyo.

“Tunamshukuru mwakilishi wetu kwani tumekuwa tukisumbuka sana. Tulikuwa tunauliza tutapata kibanda hapa kwa kituo cha Taraja lini lakini leo Mungu amemleta mwakilishi Ogugu na ametupa mabati. Tutajanga kibanda ili tuendelee kufanya kazi jinsi ilivyo ili nasi tupate riziki ya kila siku,” alisema Geoffrey Onditi, mwendeshaji bodaboda.

“Nami naomba mwakilishi aendelee kusaidia waendeshaji bodaboda wenzetu ambao hawajapata kibanda ili sote tuwe tunafurahia matunda ya mwakilishi wetu kutoka kwa serikali ya kaunti ya Kisii,” alisema Victor Ogeto, mwendeshaji bodaboda. 

Mwakilishi huyo pia aliwaomba wanakandarasi wa kutengeneza barabara za wadi yake watengeneze barabara hizo vizuri ili wakaazi wa eneo hilo waweze kunufaika.