Siku moja tu baada ya tume ya kuthibiti bei ya mafuta ghafi nchini ERC kuongeza bei ya mafuta, baadhi ya wakazi wa kaunti ya Nyamira wamejitokeza kulalamikia hali hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na baadhi ya waendeshaji magari ya umma mjini Nyamira, baadhi yao waliishtumu tume hiyo kwa hatua hiyo, hali waliyosema imeathiri pakubwa biashara zao.

"Kwa kweli hii hatua ya tume ya ERC kuongeza bei ya mafuta hasa petroli kwa shillingi nne zaidi imeathiri sana biashara ya usafiri kwa maana wengi wa wasafiri hukataa kulipa nauli zaidi kuliko ile ya awali, hali ambayo imetusababishia hasara," alisema Robert Ondieki. 

Kwa upande wake mmoja wa wauazaji mafuta ya petroli kwenye kituo kimoja cha mafuta mjini Nyamira; Vincent Mwasi, baadhi ya waendeshaji magari na pikipiki hupinga kulipa kiwango cha pesa kinachostahili kwa kulalamikia hali ya uchumi.

"Baadhi ya watu tunaowauzia mafuta hukataa kulipa pesa zaidi kwa kulalamikia hali mbaya ya uchumi, hatua ambayo imemlazimu mmiliki wa kituo hiki kupunguza bei hiyo ya mafuta kwa shillingi moja," alihoji Mwasi. 

Ikumbukwe kuwa tume ya kuthibiti bei ya mafuta nchini ERC ilisema kuwa hatua ya kuongezeka kwa bei ya mafuta nchini inatokana na hali ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa hiyo kwenye masoko ya mtaji.