Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waendeshaji pikipiki katika kituo kimoja kilichoko kaunti ya Likoni wametishia kuandamana kufuatia visa vya unyanyasaji ambavyo wanakumbana navyo kila siku wakiwa barabarani kutoka kwa wenzao wa matatu ya usafiri wa umma.

Wakiongea na mwandishi huyu, wahudumu hao wameelezea kero lao huku wakitaka maafisa wa kitengo cha trafiki katika kaunti hiyo kuwajibika vilivyo.

Haya yamejiri baada ya msururu wa visa vya ajali za pikipiki na matatu kushuhudiwa kwa mujibu wa mwenyekiti wa waendesha pikipiki eneo hilo. 

Kisa cha hivi karibuni kimetokea mapema hii leo pale mwendeshaji pikipiki amepata majeraha ya kichwa na abiria wake kuvunjika mguu baada ya dereva wa matatu kushika breki kwa dharura kwa makusudi na kupelekea ajali hiyo kwa mujibu wa aliyeshuhudia tukio hilo.

"Hao madereva wa matatu hutaka kutawala barabara yote bila kuzingatia sheria za barabarani," alisema mwenyekiti. 

Ameongeza kuwa madereva hao hufanya kusudi zaidi wanapoona maafisa wa trafiki hawapo barabarani.

"Barabara ni ya watu wote na magari yote ya usafiri zikiwemo tuk tuk na baisikeli," aliongeza mwenyekiti.

Hata hivyo ameiomba idara ya trafiki kuwasaidia kwa kuhakikisha kuwa madereva kama hao wanashtakiwa kwa kuvunja sheria.

Madai sawia na hayo yametolewa na abiria wanotumia usafiri huo wa pikipiki.