Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Picha/ ebru.co.ke]
Wafanyabiashara 11 wamefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kwa kosa la kupatikana na mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini.Washtakiwa hao walishikwa mnamo Oktoba 10, 2017 katika maeneo tofauti jijini Mombasa.Peter Chacha, Micheal Nyawa na John Mwita walitiwa mbaroni wakiwa na mifuko hiyo katika soko kuu la Kongowea.Mumo Ngangi, Timothy Mwiti, Katoi Mangi na Martin Musila walishikwa eneo la Buxton wakitumia mifuko hiyo kufunga matunda.Naye Adan Mohamed, Mwepa Jawa, Benson Munyoki na Amos Mumo walitiwa mbaroni katika eneo la Mwembe Tayari.Wote hao walikubali mashtaka hayo mbele ya Hakimu Martin Rabera siku ya Jumatano.Mwendesha mashtaka kutoka shirika la kudhibiti mazingira la NEMA Janet Alango ameitaka mahakama kuwahukumu washukiwa hao kwa kukiuka agizo la kupinga marufuku utumizi wa mifuko hiyo ya plastiki.Hata hivyo, Hakimu Rabera aliwaachilia washtwakiwa hao na kuwaonya dhidi ya kurudia kosa hilo.