Wanabiashara mjini Nyamira wamelalamika hali ya nguvu za umeme kupotea kila mara katika maeneo mengi mjini humo, jambo ambali linaathiri pakubwa biashara zao.
Kwenye mahojiano na wanabiashara hao siku ya Jumanne, mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye ni mmiliki wa chumba cha kutengeza nywele alisema hali hiyo imemsababishia hasara kubwa.
"Unajua wakati mwingine sisi hupata hasara kubwa kutokana na kupotea kwa nguvu za umeme, na tunashangazwa tatizo ni lipi," alisema Hellen Moraa.
Kwa upande wake mmiliki mmoja wa kinyozi ameitaka kampuni ya usambazaji umeme katika kaunti hiyo kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa hali hiyo inarekebishwa, huku akiongezea kuwa inawawia vigumu kulipia stima kila mwezi ilhali hamna usambazaji mzuri.
"Ombi langu kwa kampuni ya Kenya Power hapa Nyamira ni kwamba tunataka watupatie stima ya kutosha kwa maana hatutaki kushuhudia kupotea potea ovyo kwa umeme ilhali hata sisi tuko kwenye biashara na itakuwaje kwamba kampuni hiyo itataka tulipie matumizi ya stima ikiwa huduma zenyewe hatupati," alisema Clifford Ongwae.