Wafanyabiashara katika soko kuu la Daraja Mbili katika kaunti ya Kisii wametishia kufanya maandamano iwapo soko hilo halitakarabatiwa na kujengwa kufikia viwango vya kuridhisha.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mrundiko wa uchafu, miundo msingi mibaya, na ukosefu wa vyoo vya kujiasaidia katika soko hilo lililoko viungani mwa mji wa Kisii kitakuwa chanzo kikuu cha wafanyabiashara hao kudhamiria kuchukua hatua hiyo.

Baadhi ya wafanyabiashara hao ambao waliongea na huyu mwandishi walilalamikia mazingira mabovu ya kufanyia biashara, huku miongoni mwao wakitaja barabara mbaya za kuingia sokoni humo kama jambo ambalo wanadai limewasababishia hasara, kwa vile magari mengi hushusha mizigo mbali, na kuwalazimu kuwatumia wabeba mizigo ambao hutoza pesa nyingi za kubeba bidhaa hizo.

Gladys Kerubo ambaye ni muuzaji wa sukumawiki na kabeji aliskitikia hali hiyo ambapo alisema kuwa wengine wao huwa wanakula chakula chao kwenye mikahawa iliyoko karibu na soko na huenda wapate maradhi kama ya kipindupindu.

“Namwomba gavana wetu Bwana James Ongwae na serikali yake kutimiza ahadi aliyotoa akiingia kwenye mamlaka; tujengee vibanda vya kujikinga mvua ili tufanya biashara yetu bila shida,” alirai mfanyabiashara huyo.

Naye Julius Mokaya ambaye huleta viazi kwa gari na kuuzia wafanyabiashara wengine wa rejareja alimtaka Ongwae kushughulikia barabara za kuingia sokoni ili kurahisisha uchukuzi wa mazao na bidhaa kwenye soko.

Kwa mama Mary Keera, ambaye anauza nyanya alitaka kufunguliwa kwa vyoo vipya ambavyo vimekamilika, na bado havijaanza kufanya kazi, akiongeza kusema kuwa imekuwa vigumu kwao kufanya biashara na hawana mahali pa kujisaidia wakati wa haja.