Wafanyabiashara katika soko la Marikiti wameiomba idara ya usalama kupeleka maafisa zaidi wa usalama eneo hilo ili kushika doria.
Wanasema tangia wiki hii kuanza, kumekuwa na ongezeko la wateja wanaonunua bidhaa mbalimbali huku idadi ya watu wanaozuru mjini ikiongeka mara dufu, jambo ambalo wanasema linahitaji kufuatiliwa kwani wengine huenda wakaanza kutekeleza vitendo viovu kama vile wizi.
Musa Hajj, mfanyabiashara wa soko hilo anasema mnamo Jumatatu, mama mmoja aliporwa kibeti chake katika soko hilo pasi kujua, huku kilo zaidi ya themanini za nyama na matumbo zikiibwa katika soko hilo kutokana na idadi kubwa ya watu wanaozuru.
Anasema maafisa walioko kwa sasa hawatoshi sababu ya ukubwa wa soko hilo pamoja na milango mingi ya mjengo wa soko hilo ambalo kwa mara mwingi zaidi ya asilimia hamsini ya wakazi wa kisiwani Mombasa huenda na kununua bidhaa mbalimbali ikiwemo mboga hususani nyama kutokana na bei nafuu wanazotoza wateja wao.
Kwa upande wake mfanyabiashara mwingine Kennedy maarufu kama 'Mbabazi' aliyeibiwa nyama katika soko hilo, kila wakati wa sherehe mbalimbali za sikukuu zinapowadia huwa kuna haja ya idara ya usalama kuimarisha usalama bila hata wafanyabiashara kulalama.