Wafanyabiashara katika soko la Marikiti wamempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kulikarabati soko hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyabiashara hao wamesema wanaimani kuwa watapata wateja wengi kwani soko hilo sasa limepata sura mpya, ikilinganishwa na hapo awali ambapo lilikuwa na mazingira machafu.

Wafanyabiashara hao ambao walifurika sokoni humo siku ya Ijumaa ili kujua nafasi walizotengewa, walisema kuwa wanamatumaini makubwa kuwa sura hiyo mpya itawasaidia kupanua biashara zao.

Ali Mwanzia, anayefanya kazi ya kuuza mboga alisema kuwa kwa sasa soko la Marikiti limebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuezekwa kwa paa mpya lililokuwa likivuja.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Nicholas Menza, ambaye alisema kuwa wanatarajia biashara kuimarika kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa soko hilo, Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa soko hilo litapanuliwa vilivyo ili kutoa nafasi kubwa kwa wafanyabiashara wanaopania kuendeleza biashara zao.

Rais Kenyatta aidha aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa soko la nyama litakamilika mwezi Disemba mwaka huu.

Wafanyabishara wametengenezwa sehemu ambazo watakuwa wakiweka bidhaa zao kando na kukarabatiwa kwa mabomba ya kusafirishia maji taka pamoja na kujengwa kwa vyoo.