Kufuatia hali ya kupotea kwa nguvu za umeme kwenye maeneo mengi katika kaunti ya Nyamira, baadhi ya wafanyabiashara wamejitokeza kulalamikia hali hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano ya kipekee mapema Jumatano, mmiliki wa kiwanda cha kuokea mikate cha NYASTA LTD mjini Nyamira John Moriasi alisema kuwa hali ya kupotea kwa nguvu za umeme inaathiri sana biashara yake. 

"Kuna kiwango cha mikate sisi hutarajia kuhoka kila siku, lakini kutokana na hali hii ya nguvu za umeme kupotea kila mara, idadi hiyo ya mikate ya kuhokwa hupungua hata zaidi," alisema Moriasi.

Moriasi aidha aliitaka kampuni ya usambazaji umeme nchini KPLC tawi la Nyamira kurekebisha hali hiyo kwa haraka ili kuwapunguzia wafanyabiashara hasara zaidi. 

"Ni sharti kampuni ya Kenya Power huku Nyamira iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa inarekebisha tatizo hili kwa maana biashara zetu zinaendelea kuathirika pakubwa huku mahitaji ya mikate ikiwa nyngi," aliongezea Moriasi. 

Kwa upande wake James Rori ambaye ni muuzaji maziwa kule Nyabite kwa kutumia jokovu, alilalamikia kuwa iwapo hali hiyo itaendelea kushuhudiwa kwa juma moja lijalo, itawalazimu wafanyabiashara kuandamana. 

"Kama kuna watu wanaoathirika na hali hii ya kupotea nguvu za umeme ni sisi tunaouza maziwa na unajua majokovu yetu yanategemea sana nguvu za umeme ili kuhifadhi maziwa na kutokana na hali hii sisi tumepanga kuandamana ili kuwasilisha malalamishi yetu," alisema Rori.