Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia agizo la waziri wa barabara na kazi za umma kwenye serikali ya Kaunti ya Nyamira Janet Komenda la kuwataka wafanyikazi wa idara yake kufanya kazi zaidi ya masaa ya kazi yaliyotengwa, sasa wafanyikazi wa idara hiyo wamejitokeza kuchangamkia hatua hiyo.

Akiwapongeza wafanyikazi hao wakati alipozuru sehemu mbalimbali za barabara zilizokuwa zikikarabatiwa siku ya Jumatano, Komenda alisema kuwa hatua hiyo itasaidia barabara kumalizika kwa wakati mwafaka, huku akiongeza kuwahimiza wafanyikazi wa idara hiyo kuendelea kuripoti kazini mapema.

"Nina furaha kuwa wafanyikazi wa idara yangu, wamekuwa wakifanya kazi zaidi ya masaa ya kazi na kwa kweli tumeshuhudia kumalizika kukarabatiwa kwa barabara mbalimbali kwa wakati ili watu wasiwe wakisema kuwa serikali ya kaunti hii inaendelea kuzembea kumaliza ujenzi wa barabara," alisema Komenda. 

Komenda aidha aliwaonya vikali wanakandarasi wanaozembea kazini kwa kutomaliza kandarasi zao kwa wakati, akisema kuwa wasipojukumika katika utendakazi wao atawachukulia hatua zakufutilia mbali leseni zao za utendakazi.

"Kwa kweli sijaridhishwa na utendakazi wa baadhi ya wanakandarasi, na ni onyo kwao kuwa sharti wawajibikie majukumu yao kazini, na kama hawatazingatia hilo, nitalazimika kufutilia mbali leseni zao zakuhudumu," alihoji Komenda.