Wakaazi wa mji wa Nakuru na viunga vyake huenda wakakosa huduma za maji iwapo wahudumu katika shirika la maji la Nakuru NAWASCO watagoma katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Maafisa wa muungano wa wafanyikazi wa kaunti nchini, Kenya County Government Workers Union (KCGWU) tawi la NAWASCO Jumatano walitoa onyo hilo wakimshtumu mmoja wa wakurugenzi wanayedai ananuia kumwondoa mamlakani mkurugenzi mkuu James Ng’ang’a kupitia mahakama.
Akizungumza afisini mwake Jumatano, Francis Makokha ambaye ni katibu wa muugano huo, alimshtumu Geofrey Asanyo ambaye kipindi chake cha kuhudumu kama mkurugenzi mkuu kiliisha na sasa anadaiwa anashinikiza kuondolewa kwa Ng’ang’a kwa misingi kuwa aliwaajiri Chege Mwangi na Milicent Akinyi katika afisi hiyo bila kutumia utaratibu unaofaa.
Kwa upande wake mwenyeiti wa muungano huo Zephaniah Nyambane, ni kuwa Ng’ang’a ameimarisha hali ya utendakazi katika kampuni hiyo ikiwemo kuangazia swala la mishahara, ushirikiano mwema kati ya wafanyikazi mbali na huduma za maji na majitaka zilizoimarika huku akiitaja hatua ya Asanyo kuwa hawatakumbatia kamwe.
“Bw Ng’ang’a amefanya mabadiliko mengi katika NAWASCO na njama ya Bw Asanyo hatutaitikia kamwe,” Zephania alisema.