Wafanyibiashara katika Soko la Kongowea wamelalamikia hali mbaya ya barabara katika soko hilo hasa wakati huu ambapo mvua kubwa inaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Wakizungumza sokoni humo siku ya Alhamisi, wafanyibiashara hao walisema kuwa mvua inayoshuhudiwa katika eneo hilo inaathiri biashara zao kwa kuwa wateja huogopa kuenda kununua bidhaa katika soko hilo kwani huwa kumejaa matope.
Peter Nyagah, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa wafanyibiashara katika soko hilo, alisema kuwa wamekuwa wakiahidiwa kuwa barabara hizo zitaboreshwa kwa kukarabatiwa ili kutoa fursa kwa wafanyibiashara kutekeleza kazi zao pasi na ugumu wowote, lakini swala hilo likaingizwa siasa.
Nyagah alidai kuwa viongozi pia wameingiza siasa katika swala la upanuzi wa baadhi ya sehemu za kufanyia biashara.
“Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kukarabati barabara hizi lakini kwa sasa zimejaa matope na maji. Hali hiyo imewafanya wateja kukwepa sehemu hii jambo ambalo linatunyima riziki yetu ya kila siku,” alisema Nyagah.
Ali Kifalu, mfanyibiashara, alisema wao hupata hasara kunaponyesha kwa vile wateja wao hununua bidhaa kutoka wafanyibiashara wanaohudumu katika maeneo yasiyokuwa na matope.
Mfanyibiashara huyo ameitaka serikali kuu kushughulikia swala hilo kwani msimu wa mvua umeanza na anahofia kupoteza wateja.