Wafanyibiashara katika Soko la Kongowea, wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa wanasafisha soko hilo ili kuepukana na mkurupuko wa maradhi ya kiafya hasa msimu huu wa mvua.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na Katibu wa Chama cha Wafanyibiashara wa Soko la Kongowea Peter Nyaga, wafanyibiashara hao wamesema kuwa serikali ya kaunti hiyo inafaa kutuma maafisa wake kusafisha soko hilo hata mara tatu kwa wiki ili kuliweka katika mazingira safi.

Akizungumza siku ya Jumapili na wanahabari sokoni humo, Nyaga alisema kwamba hali ya mazingira duni ya soko hilo, pamoja na kuwepo kwa mirundiko ya taka, imechangia kuwepo na biashara duni, hali ambayo inayochangia kudorora kwa uchumi wa nchini.

“Tunaiomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa inasafisha soko la Kongowea ili kuona kuwa maswala ya mazingira bora yanaangaziwa, kwani soko hili linatumiwa na wananchi wa Afrika mashariki. Iwapo litabaki na mazingira mabaya, basi huenda Wizara ya Afya ikalifunga,” alisema Nyaga.

Wafanyibiashara hao wameshinikiza viongozi wa Kaunti ya Mombasa kukarabati masoko ya kaunti hiyo ili kuona kuwa biashara ya wachuuzi inafanikishwa mjini humo.