Kufuatia mzozo wa umiliki wa soko la Keroka kati ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii kuendelea kushuhudiwa kwa muda sasa, wafanyabiashara wa mji huo wanaoendelea kukadiria hasara na kuwataka magavana wa kaunti hizo mbili kumaliza utata huo.
Akihutubia wanahabari siku ya Alhamisi, msemaji wa wafanyabiashara hao John Omwenga alisema kwamba yafaa gavana wa kaunti ya Nyamira na mwenzake wa Kisii waitishe mkutano wa viongozi ili kusuluhisha mzozo huo wa umiliki wa mji wa Keroka.
"Naona kwamba magavana wa kaunti hizi wasipoitisha mkutano wa pamoja utakaowahusisha viongozi wa kisiasa, basi ni kama tatizo hili la mpaka litaendelea kuwa baya zaidi na sisi ndio tutakaoumia," alisema Omwenga.
Omwenga aidha aliongeza kwa kusema kuwa iwapo kaunti hizo mbili hazitaafikia suluhu la mzozo huo wa kimpaka kwa haraka, yafaa ushuru usikusanywe hadi pale suluhu litakapopatikana.
"Sioni haja ya maafisa wa ukusanyaji ushuru waendelee kutoza kodi hapa keroka ilhali suluhu la mzozo huu halijapatikana, na ndio sababu sisi wafanyabiashara tunaona ni heri ukusanyaji ushuru usitishwe hadi mwafaka wa tatizo hili upatikane.," aliongezea Omwenga.