Wafanyibiashara wa bidhaa za rejareja katika eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, wamekosoa mradi wa Mwangaza Mitaani uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta siku kadhaa zilizopita.
Wafanyibiashara hao walidai kuwa serikali bado haijafanya juhudi kuimarisha usalama.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne, wafanyibiashara hao walisema kuwa hata baada ya kuwekwa kwa taa hizo, bado wakaazi katika eneo hilo wanaendelea kuporwa nyakati za usiku na watu wanaozurura sehemu husika wakiwavamia wapita njia.
Wafanyibiashara hao wameitaka serikali kuweka askari wa kushika doria usiku ili kukabili tatizo hilo, kwani majambazi wamekuwa wakitekeleza uovu wao licha ya kuwepo kwa taa hizo.
“Tunashukuru kwa taa hizi kwa kuwa zinasaidia upande wa biashara wakati wa usiku. Lakini kuhusiana na mambo ya usalama, sioni mabadiliko kwa sababu hata jana watu wanne walivamiwa walipokuwa wakitembea na kuibiwa simu zao,” alisema mfanyibiashara mmoja.
Walidai kuwa askari ambao hushika doria katika sehemu hiyo ni wachache na hawawezi kudhibiti eneo zima.
Eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, ni moja kati ya maeneo yaliyokithiri na uhalifu, ambapo vijana huvamia wapita njia nyakati za usiku na kuwapora bidhaa zao.
Idara ya usalama katika kaunti hiyo imekuwa ikifanya msako wa mara kwa mara sehemu hiyo na kuwakamata vijana wanaohusishwa na visa hivyo.
Uzinduzi wa mradi wa Mwangaza Mitaani ulilenga kuimarisha bishara pamoja na kuinua kiwango cha usalama Mombasa.