Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Siku chache tu baada ya Gavana wa Kisii kudai kuwa kiwango cha ushuru walichokuwa wakikusanya kimepungua, jumuia ya wafanyabiashara katika kaunti hiyo wamepinga madai hayo na kusema kuwa ufisadi miongoni mwa maafisa wa kukusanya kodi ndio chanzo kikubwa cha ushuru kupungua.

Wafanyibiashara hao walidai kuwa kuna maafiasa wa kaunti ambao huwapokeza wafanyibiashara risiti bandia na pesa ambayo wanakusanya kila siku huishia mifukoni mwao na kunyima kaunti hela ambazo inahitaji sana ili kufanikisha miradi yake.

Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara mjini Kisii siku ya Jumanne, mwenyekiti wa wafanyibiashara katika kaunti hiyo, Walter Nyakundi alimtaka Gavana James Ongwae kuwajibikia kazi yake kwa kuwafurusha kazini maafisa fisadi ambao wanahudu kwenye kaunti.

Alidai kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara mjini Kisii ambao hawalipi kodi ya kila siku na wengine hawajahi kupata leseni kwa kile alichodai kuwa mapendeleo.

"Baadhi ya wenye biashara hapa mjini ni rafiki za gavana na maafisa wa idara za kaunti na huwa hawalipi kodi wala hawajakata leseni ya biashara kwa muda wa miaka mitatu sasa. Hiyo ni mojawapo ya visa vinavyochangia ukosefu wa uwajibikaji," alisema Nyakundi.

Alionya kuwa iwapo serikali ya kaunti haitawajibikia majukumu yake huenda wafanyabiashara kutoka Kisii wakasusia kulipa kodi.

"Sharti maafisa wa kaunti waongoze kwa kuwa na mfano mwema kuliko kuendelea kuwa na mapendeleo ilhali kila mmoja anahitaji kuchangia ili kuiendeleza kaunti yetu ya Kisii," alisema Nyakundi.