Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Licha ya samaki kupanda bei, bidhaa hiyo imeanza kuadimika mjini Kisumu kwanzia siku za hivi majuzi huku wachuuzi wakipanga foleni kwenye vuo za mto Victoria.

Samaki waliyouzwa Sh280 awali sasa wanauzwa kwa bei ya Sh350 kwa kila kipimo cha kilo moja, kwa mujibu wa Milka Okoyo Nyangweso ambaye ameifanya biashara hiyo kwa miongo miwili sasa, hali hiyo imesababishwa na ongezeko la wanunuzi wa jumla kutoka nje.

Nyangweso alisema kuwa wavuvi katika vuo nyingi za ziwa Victoria wametegemea sana wanunuzi kutoka nje ambao huchukua bidhaa hiyo kwa wingi.

''Samaki wanachukuliwa kwa kiwango kingi sana na wanunuzi wa jumla kutoka nje, sasa sisi tunaotegemewa na wanunuzi wa kawaida, kiwango chetu ni kidogo na bei ni ile ya juu kwa kila kilo,'' alisema Nyangweso aliyekuwa akiongea na Mwandishi huyu siku ya Jumatatu.

Aidha, alidokeza kuwa hali hiyo inafanya wateja kung'ang'ania ununuzi wa samaki uvuoni huku wengine wakihitajika kusubiri hata kwa muda zaidi wa masiku.

''Usipofika pale mapema na kupiga oda utalazimika kusubiri muda mrefu hata siku mbili kabla hujapata samaki,'' alisema mchuuzi huyo.

Samaki ni bidhaa inayotegemewa sana katika kanda wa Nyanza kama chakula na kitega uchumi. Walioanza kufanya biashara hiyo zamani wamejiendeleza kimaisha.

Chombo cha kubebea samaki. Wachuuzi wa samaki mjini Kisumu wameelezea wasiwasi yao kutokana na ongezeko la bei na uhaba wa bidhaa hiyo kwa sasa.