Wafanyibiashara katika eneo la Mama Ngina kaunti ya Mombasa wanahofu kutokana na madai kwamba eneo hilo wanalofanyia biashara limenyakuliwa na mtu binafsi.
Hii inatokana na ripoti iliyotolewa na kamati ya umma ya uwekezaji PIC inayosema kuwa eneo hilo la Mama Ngina pamoja na lile la ngome ya Fort Jesus yamenyakuliwa na mabwanyenye.
Akiongea na mwandishi wetu katika eneo hilo Jumatano, Suleiman anayefanya biashara ya kuuza vinywaji alisema kuwa amefanya biashara hapo kwa miaka mingi kukimu familia yake.
“Kama hili eneo limenyakuliwa basi sisi wafanyabiashara wadogo hatuna pa kwenda, hapa tunahudumia wageni wengi kutoka mbali na hili ndio eneo tunalopata kipato chetu,” alisema Suleiman.
Mama Ngina ni moja kati ya maeneo makubwa yaliyo kando ya fuo ya bahari Indi ambapo watu wengi hupenda kuzuru na kujipumzisha huku wafanyabiashara wakiuza bidhaa mbalimbali.
Baadhi ya bidhaa wanazouza ni pamoja na vinywaji vya kiasili kama maji ya madafu, mihogo karanga na vyakula vya kila aina hasa kwa wageni wanaozuru eneo hilo kutoka maeneo mbalimbali.