Wafanyibiashara wanaouza tende wametakiwa kupunguza bei ya bidhaa hiyo mwezi huu wa Ramadhan.
Baraza la Maimam na Wahubiri nchini CIPK, imesema kuwa hatua hiyo itakuwa jambo la busara kwa sababu Rais Uhuru Kenyatta alitoa maagizo hayo wakati wa Sherehe za siku ya Madaraka katika uwanja wa Afraha huko Nakuru.
“Nawasihi wafanyibiashara wa tende kupunguza bei za bidhaa hiyo ambayo huitajika mno wakati wa Ramadhan,” alisema Katibu mtendaji wa Baraza la CIPK Sheikh Mohammed Khalifa.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Mombasa, Sheikh Khalifa aliwataka Waislamu nchini kuhubiri amani na utangamano.
Alisema kuwa mwezi huu unapaswa kuwa wa mwanzo mpya na utangamano kwa watu binafsi na mataifa yote kwa jumla.
"Kando na kufunga mwezi huu mtukufu, nawaomba kujitenga na maovu na kulinda amani yenu huku mkifata sheria,” alisema Sheikh Khalifa.