Siku moja baada ya mkurugenzi mkuu wa Halmashauri ya Bandari nchini KPA Gichiri Ndua pamoja na maafisa wengine kusimamishwa kazi, wafanyibiashara mjini Mombasa wanaendelea kutoa hisia mseto kutokana na hatua hiyo.
Baadhi ya wafanyibiashara hao ambao wengi wao ni wauza magari miongoni mwa bidhaa zingine zinazopitishwa bandarini humo, walisema kuwa wamefurahishwa na hatua hiyo.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini humo, Charles Otieno, mfanyibiashara, alisema kuwa anaunga mkono hatua hiyo lakini akasisitiza kwamba huo ni mwanzo tu.
“Hiyo ni hatua nzuri lakini sio mwisho wa ufisadi bandarini. Serikali sasa inafaa kuhakikisha kuwa inawachunguza vizuri wale watakaochukua nafasi hiyo,” alisema Otieno.
Wafanyibiashara hao aidha walilaumu idara ya uchukuzi nchini kwa kwa kushindwa kugundua visa vya ufisadi na kuvikabili mapema kabla ya kuenea.
“Hayo mambo ya ufisadi bandarini yamekuwepo kwa muda mrefu lakini mimi nashangaa mbona saa hii ndio wanaona kuwa kuna shida. Suluhu ya haya mambo kuisha ni idara ya uchukuzi kukaza kamba kwa sababu yeyote anayeajiriwa pale analenga kufuja pesa,” alisema mfanyibiashara mwingine.
Wakati huo huo, wafanyibiashara hao walisema kuwa halmashauri ya KRA inafaa kuchunguzwa kwa kushindwa kuzuia changamoto ya wafanyibiashara kukwepa kulipa ushuru.
Siku ya Jumanne waziri wa uchukuzi nchini James Macharia aliagiza kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya KPA, pamoja na maafisa wengine kwa madai ya kutumia vibaya afisi zao.
Hatua hiyo inakuja siku kadhaa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuongoza zoezi la kuharibu bidhaa ghushi zilizonaswa bandarini humo ikiwa ni pamoja na sukari na mchele, miongoni mwa bidhaa zingine.