Wafanyabiashara wa mboga na matunda katika soko la Daraja Mbili lililoko viungani mwa mji wa Kisii wanakadiria hasara kubwa kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo la Kisii, hali ambayo imesababisha kuharibika kwa bidhaa hizo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi ambayo ni siku kuu ya soko, mwenyekiti wa wauzaji matunda na mboga katika soko la Daraja Mbili Ernest Birundu, alitaja hali ya mazingira na uwepo wa maji kwenye eneo wanaweka mboga na matunda yao kuwa chanzo cha kuoza kwa mazao hayo.

Alishauri wizara husika ya uratibu wa mji kuzingatia miundomsingi ya soko hilo, ili waweze kuwa na vibanda safi ambamo watakuwa wakiweka bidhaa hizo na kuepuka hasara za kuzuilika kama hizo wanazoshuhudia kwa sasa.

Benson Sagini ni mfanyabiashara wa nyanya, ambaye kwa usemi wake amepata hasara ya zaidi ya shilingi elfu 10, ambapo alisema kuwa nyanya zote alizonunua siku ya Jumatatu, ziliweza kusombwa na nyingine kuoza.

Sagini alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuwajengea jumba kubwa ambalo wafanyabiashara watalitumia kuweka bidhaa zao kabla na baada ya shughuli za kibiashara.

Soko hilo limekuwa likizua hoja kila mara, hasa kunakotokea kisa kwani gavana wa Kisii Ongwae ameahidi kulijenga soko hilo mara si moja.