Wafanyibiashara wanao husika na upishi na uuzaji wa vyakula katika Tarafa ya Kabazi kwenye Kaunti ndogo ya Subukia wamepewa makataa ya majuma mawili kupata vyeti vya Afya ili waruhusiwe kuendesha biashara zao.
Afisa wa Afya anaye simamia Tarafa hiyo Reuben Gitau siku ya Ijumaa kwenye baraza la mkutano wa kuhamasisha umma kuhusu ugonjwa wa kipindupindu katika kituo cha kibiashara cha Kabazi kuwa, alisema sharti wafanya biashara wote wa nyama, hoteli, duka na kadhalika wakaguliwe afya yao ili waweze kupewa vyeti hivyo.
“Ingawa hakuna dalili zozote zimeripotiwa au kuonekana, ofisi ya afya inachukua hatua hii kama tahadhari ya kuzuia kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu. Kila mmoja azingatie usafi katika makazi au biashara yake,” alisema Chifu Gitau.
Afisa huyo aliongeza kuwa wale watakao patikana wakichuuza vyakula watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akihutubu kwenye mkutano huo, Afisa wa utawala katika Tarafa ya Kabazi Ann Mitema aliwahimiza wakaazi wote kushirikiana na Maafisa wa afya ili kuzuia kuzuka kwa ugonjwa huo pamoja na mengineyo yanayotokana na maji machafu.
“Ofisi yangu itahakikisha kuwa masharti na sheria za afya zinafuatwa na kutekelezwa kikamilifu. Nawasihi wakaazi wote wa Kabazi kuripoti haraka dalili za ugonjwa huo ili hatua mwafaka ziweze kuchukuliwa kabla ya maafa yoyote,” alisema afisa Mitema.
Afisa Gitau alisema muda wa majumaa hayo mawili umetosha kwa wahudumu wote kufuata agizo hilo na wale ambao hawatatimiza maagizo hayo hawataruhusiwa kuendesha biashara zao.