Mwenyekiti wa muungano wa wafanyibiashara wa kuagiza magari mjini Mombasa Peter Otieno, ameyapinga madai ya mshirikishi wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa, kuwa wanajihusisha na biashara haramu ya ulanguzi wa mihadarati.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye kikao na waandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Otieno alisema kuwa madai ya Marwa hayana ukweli wowote, kwani wanachama wa muungano huo wanatekeleza biashara yao kuambatana na sheria, na kuwa hawajawahi husika na ulanguzi wa mihadarati mjini humo.

“Sisi tunayaagiza magari kutoka mataifa ya nje kama Japan. Nashindwa magari haya yanatoka Japan yakiwa na mihadarati ndani? Na ikiwa dawa hizi zinapakiwa hapa Bandarini, nani analipia shughuli hiyo?” aliuliza Otieno.

Mwenyekiti huyo sasa amemtaka Marwa kuwalaumu maafisa wa usalama kwa kukithiri kwa biashara ya ulanguzi wa dawa za mihadarati katika ukanda wa Pwani, badala ya kuwalimbikizia lawama.

Hata hivyo, Otieno alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na idara ya usalama mjini humo ili kuwakabili wanaotekeleza biashara hiyo.

Aliahidi kuwachukulia hatua kali wanachama wa muungano huo ambao watapatikana na hatia.

Mapema mwezi huu, Marwa aliwaagiza maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi katika maduka yanayofanya biashara ya kuingiza na kuyauza magari, kwa madai kuwa yanapakia dawa za mihadarati katika tairi za magari na kisha kuziuza kwa wakaazi.