Wafanyikazi wa kuuza makaa katika eneo la Majengo mjini Mombasa wameitaka serikali ya kaunti kuingilia kati na kusitisha hatua ya wao kuhangaishwa na baadhi ya mabwanyenye katika eneo hilo.
Wafanyibiashara hao walidai kuwa kwa muda sasa wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani wana wasiwasi kuhusu hatma ya biashara zao, baada ya kuanza kupokea vitisho kutoka kwa mabwanyenye hao.
Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumamosi, wafanyibiashara hao walidai kuwa watu hao walishirikiana na maafisa wa manispaa, kuvuruga biashara zao usiku wa kuamkia siku ya Jumamosi kabla ya kubeba bidhaa zao kwa nguvu.
“Walikuja na tinga wakati wa usiku na kubomoa vibanda vyetu bila taarifa kisha wakachukua makaa yetu na kuondoka nayo. Tulipoamka asubuhi, tulipata wameanza kuweka vikingi katika eneo tunalofanyia biashara yetu,” alisema Kombe Katoi, mmoja wa wafanyibiashara hao.
Wafanyibiashara hao walisema kwamba wamefanya biashara ya kuuza makaa katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20, na hiyo ndio imekuwa shughuli wanayoitegemea kujikimu kimaisha.
Walisema kuwa wameshangazwa na hatua hiyo huku wakiongeza kuwa wana vibali vinavyohitajika kuendesha biashara hiyo, na pia wamekuwa wakilipa kodi kama kawaida.
“Tukileta mzigo kutoka shambani, huwa tunalipa fedha katika kila kituo tunachopitia na hata tukifika hapa, pia tunatoa malipo kwa manispaa. Kibali cha kufanyia biashara pia tuko nacho kwa hivyo hakuna sababu ya kuhangaishwa,” alisema Rajab, mfanyibiashara.
Sasa wamesema kuwa huenda hiyo ni njama ya matajiri hao kuwafurusha ili waanzishe biashara zao.
Wafanyibiashara hao wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuingilia kati na kubaini iwapo maafisa wa manispaa waliohusika na kisa hicho walitumwa au ni baadhi tu waliolipwa na mabwanyenye hao kutekeleza uovu huo.
Biashara ya makaa mjini Mombasa hutegemewa na watu wengi hasa wafanyibiashara wa kupika vyakula kutokana na gharama yake kuwa nafuu.