Wafanyabiashara katika mji wa Kisii Mapema leo (Alhamisi) wameandamana katika barabara za mji huo kulalamikia unyakuzi wa eneo la kufanyia biashara maarufu katika mji huo kama 'Market’.
Akiongea kwenye mahojiano na Mwandishi huyu wa Habari, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa 'Open Air Market' mjini Kisii Elijah Ombongi amedai kuwa wamepata karatasi za arifa ambazo ziliamurisha kuwa wamepewa siku saba kuhama eneo hilo liweze kufanyiwa ujenzi na mwekezaji binafsi, jambo ambalo limewatamausha wengi wao.
Ikumbukwe kwamba haya ni maandamano ya pili kuhusu eneo hilo la soko kwani waliandamana mwanzo wa mwaka huu wakitaka mwekezaji huyo kuzuiwa kuendeleza eneo hilo.
Wafanyibiashara hao walikuwa wakiongozwa na Mwakilishi wa Wadi ya Kisii mjini Wilfred Monyenye ambaye tayari alikuwa ametangulia kuenda kumwona Gavana kujadili suala hilo.
Dinah Kebwaro ambaye ni mmoja wa waandamanaji hao alilalama akisema kuwa Serikali ya Kaunti inahitaji kuwajengea mahali pa kufanyia biashara zao kabla ya kutolewa walioko kwa sasa.
“Sina kazi nyingine mbali na biashara hii ya matunda na mboga kwa hiyo tunamtaka Waziri wa Ardhi pamoja na Gavana wetu James Ongwae kuingilia kati na kutatua mzozo huu haraka iwezekanavyo,” alihoji Kebwaro.
Hata hivyo hawakuhutubiwa na Gavana kwani Maafisa wa Polisi walikuwa chonjo mlangoni wa kuingia ofisi ya Gavana tayari kuwakabili waandamanaji hao.