Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanawake wa kuuza nguo za mitumba katika mji wa Kisii wamemtaka Gavana wa kaunti hiyo Bwana James Ongwae kupunguza kiwango cha ada ambayo wao hutozwa kila siku na zile wanazo lipa ili kupewa leseni ya kuhudumu kwa mwaka.

Wafanyibiashara hao walisema kuwa serikali ya kaunti huwa inawatoza kiwango kikubwa mno ikilinganishwa na hela ambazo wanatumia katika shughuli ya kununua bidhaa zao.

Aidha, waliwalaumu baadhi ya maafisa wa kaunti ambao hukusanya ushuru kwa kujihusisha katika ufisadi.

Akiongea kwa niaba ya wanawake hao siku ya Alhamisi kwenye kikao cha kuwasilisha malalamiko yao kwa waandishi wa habari katika makao ya idara ya mawasiliano mjini Kisii, Bi Jane Moraa ambaye ni mwenyekiti wa jumuia hiyo ya wauza mitumba alidai kuwa serikali ya kaunti imeanza kuwanyanyasa kwa kuongeza hela za ushuru kila mara na kufanya maamuzi bila kuwahusisha.

Mfanyibiashara huyo alimtaka gavana kutafuta suluhu la kudumu kuhusiana na kuongezeka kwa ada ya kupata leseni ya biashara.

“Sharti gavana awahusishe wadau katika sekta ya biashara anapofanya maamuzi muhimu. Sio haki kufanya maamuzi bila kutuhusisha na sisi ndio washika dau kwenye sekta hii. Tunamtaka gavana kuliangalia suala hili kwa dharura,” alisema Bi Moraa.

Wafanyibiashara hao pia waliitaka serikali kutengeneza kamati maalumu ya kushughulikia masuala yanayohusiana na biashara na wafanyibiashara katika miji yote ilioko katika kaunti ya Kisii.