Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafanyibiashara wanaoagiza na kutoa mizigo mjini Mombasa wamelalamikia kunyanyaswa na maafisa wa polisi wa trafiki wanaoshika doria katika daraja la Nyali.

Wakizungumza siku ya Alhamisi katika kongamano la wafanyibiashara mjini Mombasa, wafanyibiashara hao walidai kuwa maafisa wa polisi wanaohudumu katika daraja hilo huwalazimu kutoa hongo, jambo linalowasababishia hasara.

“Hata kama huna hatia unalazimishwa kutoa rushwa. Usipotoa, unazuiliwa kupita kisha baada ya kupoteza muda unaruhusiwa kuondoka,” walisema wafanyibiashara hao.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Mohammed Maalim, ambaye pia alihudhuria kongamano hilo, aliwataka wafanyibiashara hao kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kukubali mizigo yao kukaguliwa barabarani.

Maalim alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti visa vya uhalifu.

“Nawasihi mshirikiane na maafisa wa polisi ili tulinde usalama wa kila mmoja na kuwabaini wanaondesha biashara haramu,” alisema Maalim.

Maalim pia aliwahakikishia usalama wafanyibiashara hao.