Baada ya kuliangazia soko la Nyakongo lilioko wadi ya Sensi kaunti ya Kisii mnamo tarehe kumi mwezi huu, sasa matayarisho kabambe yanaendelea ili kulifungua soko hilo haraka iwezekanavyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mipango hiyo ambayo kwa sasa inaendelea ni pamoja na kukarabati barabara zinazolizunguka soko hilo ili kuwapa wafanyabiashara usafiri mwafaka.

Mwakilishi wa wadi ya Sensi Onchonga Nyagaka amesema matayarisho hayo ni ya mwisho kwa maandalizi ya ufunguzi.

“Wanaendelea kutengeneza hizo bararabara, niliongea na wizara ya leba, na soko hilo litafunguliwa baada tu ya kukamilika kwa ukarabati wa barabara hizo,” alisema Nyagaka.

Wafanyabiashara wameonyesha furaha yao wakisema imani yao imerejea.

“Tuko na furaha sana ndiposa tumesimama hapa kuona vile wanatengeneza barabara kwani zimekuwa na matope hata mtu hawezi pita lakini sasa unaeza pita hata kwa ndala ziko sawa kabisa hata wenye duka ambao tunatumia rukwama sasa itakuwa rahisi kupita," alisema mfanya biashara mmoja.

“Soko hili letu limekawia siku nyingi tumengoja lakini mwishowe tunaona litafunguliwa. Matractor ziko hapa barabara ni smart pia sasa mvua haitakuwa inatusumbua, soko letu mpya litatufaidi pakubwa haswa sisi wafanyabiashara wadogowadogo,” aliongeza mfanyabiashara huyo.

Sasa wafanyabiashara hao wana matumaini kamili na wanasubiri siku hiyo kwa hamu kubwa. Pia wameahidi kulitumia soko hilo vizuri kwa manufaa yao wenyewe.