Wafanyibiashara katika kaunti ya Nakuru wamemtaka Gavana wa Jimbo hilo Kinuthia Mbugua kuhakikisha kila kaunti ndogo imepata vyombo vya kisasa vya kukabiliana na majanga ya moto.
Wafanyibiashara pamoja na wakazi mjini Molo wamesema eneo hilo limeshuhudia mikasa mingi ya moto, ambapo mali ya thamani kubwa imepotezwa.
Wamesema kuzukapo mikasa sampuli hiyo wananchi hutegemea zima moto kutoka kwa kampuni ya mbao ya Timsales, iliyoko Elburgon kwa shughuli za ukoaji.
Wameuliza gavana Mbugua kutekeleza ahadi yake katika makadirio ya mwaka huu wa kifedha, ikizingatiwa kwamba eneo la Molo pamoja na barabara kuu ya Nakuru- Eldoret kumeshuhudiwa ongezeko la mikasa ya moto kama vile kuteketea kwa malori ya kusafirisha petrol yanapohusika kwenye ajali.
Aidha, wakaazi hao wamelalamikia ongezeko la visa hivyo vya moto ambavyo vimeongezeka kila kuchao, na kutaka Mbugua achukue hatua inayostahili ya kuwapa vifaa vyo kushuglikia majanga kama hayo.