Wafanyibiashara katika kituo cha kibiashara cha Kibunja kwenye barabara kuu ya Nakuru–Eldoret wamelalamikia ongezeko la ajali katika barabara hiyo.
Wanabiashara hao sasa wameitaka mamlaka ya kitaifa ya usimamizi wa barabara kuweka matuta kwenye barabara hiyo.
Wamesema kuwa visa vya watu kugongwa na magari vimeongezeka katika siku za hivi majuzi huku watu kadhaa wakipoteza maisha yao na wengi kulemaa baada ya kuhusika kwenye ajali.
Wenyeji hao ambao hufanya biashara kandokando ya barabara hiyo wamedai kuwa magari yanayoendeshwa kwa mwendo wa kasi husababisha ajali wakisema ni sharti hatua za dharura zichukuliwe ili kuepuka maafa zaidi.
“Sisi tunafanya biashara ya kuuza vyakula kama vile viazi, kabeji, karoti, miongoni mwa mazao mengine kutoka mashambani. Hatari iliyopo hapa in ongezeko la ajali katika barabara hii. Juzi tulimpoteza mmoja wetu baada ya kugongwa na lori,” alisema Mary Gitau mfanyibiashara.
Gitau amesema kwamba ongezeko la ajali linaendelea kuwatia hofu wafanyibiashara akisema wao hutegemea wasafiri kwenye barabara kuu ya Nakuru–Eldoret ambao hununua bidhaa zao na kuwawezesha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
“Kituo hiki cha kibiashara kina watoto wengi mayatima ambao wazazi wao wamepoteza maisha baada ya kuhusika kwenye ajali. Tunaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili wenyeji waepuke na mauti ya mapema.,” aliteta Steve Ondieki muuza viazi.
Akidhibitisha madhila ya wenyeji hao, Chifu wa eneo hilo Hassan Waweru amesema wafanyibiashara wanakabiliwa na hatari ya kugongwa na magari akisema afueni itapatikana pale barabara hiyo itawekwa matuta ili kudhibiti mwendo wa magari haswa malori yenye uzani kubwa ambayo huendeshwa kwa mwendo wa kasi.
Chifu Waweru amesema eneo la Kibunja limeshuhudia ongezeko la ajali huku akiuliza madereva kupunguza mwendo na kuwa waangalifu.