Muungano wa wafanyibiashara wanaoagiza bidhaa humu nchini kupitia Bandari ya Mombasa umelalamikia uhaba wa bidhaa hizo kutokana na kutozwa ushuru wa juu.
Kwenye mahojianao ya kipekee na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Mwenyekiti wa muungano huo, William Ojonyo, alisema kuwa licha ya kuandaa mikutano mingi na maafisa wa KPA na KRA wakitaka hali hiyo kuchunguzwa, hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa na Mamlaka ya utozaji ushuru nchini KRA na wasimamizi wakuu wa Bandari ya Mombasa.
Ojonyo alisema kuwa huenda hali hiyo ikaathiri biashara nchini kwani wadau na wafanyibiashara wanapanga kutumia bandari ya nchi jirani ya Tanzania kusafirisha bidhaa zao.
Muungano huo ulisema kuwa wana imani huenda hali nzuri ya kibiashara itarejea bandarini humo iwapo maafisa wa Mamlaka hiyo pamoja na wale KPA na kutoka Wizara ya Fedha watakubali ombi lao la kulainisha ushuru wanaotozwa.
"Tumejaribu kila mbinu kuzungumza na maafisa wa KRA kuhusu swala hili lakini bado hatujapata jawabu. Hata hivyo, tuko na imani kuwa suluhu la swala hili litapatikana kabla ya wafanyibiashara wetu kuhamia katika bandari za nchi jirani ya Tanzania,” alisema Ojonyo.