Muungano wa wafanyibiashara wanaoagiza magari kutoka nchi za nje umetoa wito kwa serikali na Mamalaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini KRA, kupunguza kodi ya kuagiza magari hayo.
Akizungumza na wanahabari ofisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa muungano huo, Peter Otieno alisema kuwa wamekuwa wakilipishwa ada ya juu ili kukomboa shehena ya gari inapofika katika Bandari ya Mombasa, jambo ambalo linaathiri biashara yao.
Aidha, Otieno alisema kuwa licha ya wengi wa wateja wao kufanya uamuzi wa kununua gari kutoka nchi za nje kwa kuwa bei ni ya chini ikilinganishwa na humu nchini, gari hizo zifikapo humu nchini hulipiwa ushuru wa kiasi cha juu sana.
Sasa muungano huo umetaka mkutano ufanywe baina yake, Mamalaka ya Ukusanyaji Ushuru KRA, na maafisa wa serikali ili kuweza kupata njia mwafaka wa kutatua tatizo hilo.
“Tunalipizwa ada za juu kama ushuru wa kufanya hii biashara ndio maana watu wengi wanaleta gari za magendo nchini,” alisema Otieno.