Wafanyibiashara kwenye soko la Katito wameitaka idara ya ukusanyaji wa fedha kwenye soko hilo kuwajengea soko maalumu ili waweze kufanya biashara kwa njia ya kisasa.
Wafanyibiashara hao walitaka pesa zinazokusanywa na Manispa ya eneo hilo kutumiwa katika upanuzi na ujenzi wa soko ili kuboresha mazingira katika maeneo ya biashara, na wala isiwe tu kutafuta manufaa ya ofisi bila kujali raia wanaoendeleza ujenzi wa taifa kwa kutozwa ushuru.
Mwenyekiti wa kikundi cha wafanyibiashara kwenye soko hilo cha Umoja Business Sacco Barnwell Okumu alitaka mikakati ya ujenzi wa soko hilo kuanzishwa haraka jinsi ilivyokuwa imependekezwa hapo awali.
“Soko ambazo zilianzishwa nyuma yetu zimeendelea kukua baada ya kujengwa soko maalumu ambapo wafanyibiashara wanajivunia mauzo bora kwa kumiminikiwa na bidhaa aina nyingi zinazofikishwa sokoni na wafanyibiashara kutoka maeneo ya mbali,” alisema Okumu.
Wengi walisema kuwa soko hilo linastahili kuwa na maendeleo ya kisasa ambapo ujenzi wa majumba ya biahsara na makaazi ya wafanyibiashara yanastahili kuwekwa kwenye miundo ya kisasa ili kuvutia wawekezaji kutoka katika maeneo mengine.
“Maendeleo yanayofaa yanategemea uimarishaji wa ushindani miongoni mwa wafanyibiashara. Tukipata wageni watakaoleta bidhaa zao na pia kuishi eneo hili kibiashara hakika uchumi wetu utaimarika,” alisema Benard Obara anayefanya kazi ya hoteli kwenye soko hilo.
Soko hilo ambalo liko kwenye barabara kuu ya kutoka Kisii kuelekea jiji la Kisumu lina ushindani mkali wa kibiashara kutokana na hali ya kumiminikiwa na wauzaji na wanunuzi kutoka maeneo mbali mbali katika kanda ya Nyanza na Magharibi.